![]() |
| Michael Branch alivyokuwa kipindi akicheza soka |
Mshambuliaji
wa zamani wa klabu ya Everton Michael Branch amekutwa na hatia na kufungwa jela
miaka saba (7) kwa kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya. Michael pichani
ambaye pia amewahi kuzichezea klabu za Manchester City, Wolves na Reading
alitiwa mbaroni na polisi wa jiji la Liverpool kabla ya kufikishwa mahakamani
kwa makosa mawili ambapo alikiri yote kabla ya kupewa hukumu hiyo.
Branch,
34 alikiri kuuza karibu kilo 3 za amphetamine kwa mtu mmoja katika maegesho ya
magari jijini Liverpool na pia polisi walimkuta na kilo 1 ya cocaine ambayo
inakisiwa kuwa na thamani kati ya pauni 40,000 hadi 50,000 alipopekuliwa nyumbani
kwake Merseyside mapema mwezi Julai mwaka huu.
Akihojiwa na Livepool Echo, msemaji wa The Serious Organised Crime Agency
amesema hili ni tukio kubwa kuwahi kufanywa na mtu ambaye awali alikuwa ni kioo
cha jamii (mtu wa mfano wa kuigwa). Msemaji huyo pia aliwaasa watu kuwa,
kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya na mihadarati ni tendo lililo
kinyume cha sheria na mwisho wake ni kifungo na kamwe haliwezi kumfanya mtu
kuwa tajiri au kuishi katika maisha ya umaarufu.
Branch
atakumbukwa kuwa mmoja kati ya wachezaji waliovumbuliwa na kuendelezwa na shule
ya mpira ya klabu ya Everton ambaye kwa kipaji chake alipata nafasi kwenye timu
ya wakubwa ya Everton ( maarufu kama The Toffees ) alipofikisha umri wa miaka
17 ambapo hadi anafika umri wa miaka 20 alifanikiwa kuifungia Everton mabao 3.
Wakati huo watu wengi walimtazamia kuja kuwa mmoja wa mmoja kati ya wachezaji
tegemeo wa klabu hiyo kwa siku za usoni lakini ndoto hizo zilipotea pale
aliyekuwa meneja wa timu hiyo Joe Royle alipoondoka klabuni hapo. Baada ya hapo
Branch alianza kupigwa danadana kwa kuhamishwa kwa mkopo kwenda Manchester
City, Birmingham, na Wolves kabla ya kuuzwa kwa timu ya Molineux mnamo mwaka
2000 kwa ada ya pauni 500,000.
Katika
kipindi chake alifanikiwa kufunga mabao sita (6) tu katika mechi 67 alizocheza
katika ligi akiwa Molineux na baadae alikopeshwa kwa klabu za Reading, Hull,
Bradford, na Chester. Alipofikisha umri wa miaka 28 aliachana na mpira wa ushindani
na kujiunga na klabu za Halifax na Burscough ambazo hazishiriki ligi.

No comments:
Post a Comment